Huyu Ndiyo Storyseller Asiyeshikika Zaidi Duniani
Story selling ni moja ya mbinu ya kutengeneza mauzo kwa kutumia simulizi, lengo kuu ni kuukamata na kuushika umakini (attention) ya mnunuaji.
Storyseller mzuri zaidi duniani ni yule anayetanguliza tatizo husika mapema kabisa katika simulizi lake kabla ya vitu vyengine, hii inapelekea kuishikilia hamasa na attention ya mteja wako kuendelea kuisoma hiyo simulizi. Chukulia mfano wa story hizi mbili:
Ya kwanza: Jana jioni nilienda uwanja wa taifa kutazama mechi ya simba na yanga, kwa kuwa nilikuwa na usafiri wangu binafsi niliamua kupitia mlango mkuu ule unaotazamana na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Temeke….
Ya pili: Jana jioni nilienda uwanja wa taifa kutazama mechi ya Simba na Yanga lakini kilichonistaajabisha sana na kubaki mdomo wazi ni ule msururu wa watu waliopanga foleni ya kukata tiketi ya kuingilia uwanjani bila ya kujua ya kuwa, sasa hivi unaweza….
Tuendelee sasa, kati ya mifano hiyo miwili ya juu story ipi itashikilia ‘attention’ ya watu wengi? Bila shaka ni story ya pili. Unajua siri kuu ipo wapi? Leo ni leo nitakujuza hapo chini:
Muuzaji mzuri ni yule anayetanguliza tatizo kwanza kabla ya kujieleza yeye nani na anafanya nini, hiki unakielewa kweli? Kama inakuja hivi halafu haiji, basi ondoa shaka mimi leo nipo na wewe.
Kulitanguliza tatizo kabla ya lolote ni chambo cha wateja wako kwa sababu kulieleza tatizo awali litafanya mteja wako akukumbuke kwa urahisi.
Chukulua mfano tuna madaktari wawili, wote waliulizwa swali moja ambalo ni wao ni nani?
Jibu la wa Kwanza: “Mimi ni bingwa wa magonjwa ya uzazi”
Jibu la wa Pili: “Kutokana na wakina mama wengi kusumbuliwa na changamoto za uzazi basi nimeamua kuwa daktari bingwa wa maswala ya uzazi ili kuwasaidia kwa karibu”
Hebu tuulizane mimi na wewe kama tungekuwa sisi ndio wagonjwa ‘attention’ yetu ingeshikwa na nani kati ya hao wawili?
Basi sahau yote, ila usisahau hili:
“Wateja hawataki kusikia lolote kuhusu wewe, bali wanahitaji kusikia zaidi kuhusu wao (matatizo yao)”